This archive report was first published on 28 December 2019.
Moses Kuria: Miguna Miguna Aruhusiwe Kuingia Kenya ¶
Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria amesema Miguna Miguna anafaa kuruhusiwa kuingia humu nchini akisema ni Mkenya.
Alisema Raila Odinga mwaka wa 2009 alimhakikishia Miguna Miguna ni Mkenya na kwa hivyo hafai kufungiwa kuingia humu nchini.
Alisema alikuwa amemwandikia Raila akimfahamisha kuwa Miguna alikuwa ni raia wa Canada na hivyo kuibua maswali kwa nini alifanya kazi kwenye afisi yake.
Wakati huo, Raila alikuwa akihudumu kama waziri mkuu ndani ya serikali ya nusu mkate iliyoundwa kati yake na Mwai Kibaki baada ya machafuko ya uchaguzi wa urais wa 2007.
"Nilimwandikia aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo Raila Odinga nikimjulisha kulikuwa na raia wa Canada aliyekuwa akifanya kazi katika afisi yake kwa jina Miguna Miguna," alisema Kuria.
Alisema suala la uraia wa Miguna lilikamilika baada ya katiba ya 2010 na kwa hivyo Miguna anafaa apewe pasipoti yake.
Alisema Miguna alikuwa amejipata pabaya baada ya kumuapisha Raila Odinga kama rais wa umma mnamo Januari 30, 2018 baada ya utata kuhusu uchaguzi wa urais wa 2017.
Alisema Miguna alikuwa amebadilisha uraia wake kabla ya katiba ya 2010 na kulinga na sheria ya wakati huo hilo lilimaanisha alipoteza uraia wa Kenya.
Alisema Miguna hata hivyo amepuuza msimamo huo na kutaja anayofanyiwa na serikali kama dhuluma kutokana na msimamo wake mkali kuhusu maovu ya viongozi.
Alisema Miguna ametangaza kurejea nchini tena.