This archive report was first published on 27 December 2019.
Garissa: Wauza Miraa Watekwa Nyara na Al-Shabaab ¶
Polisi mjini Garissa wameanzisha juhudi za kuwaokoa Wakenya wawili wanaoaminika kutekwa nyara na wanachama wa kundi la al-shabaab.
Watu wawili hao, Abdulahi Isaack Harun na Abdi Hassan Ilkaase walitekwa nyara Alhamisi, Disemba 26, saa moja asubuhi wakipeleka miraa hiyo Liboi.
Polisi walisema wawili hao walikuwa wakisafirisha miraa hiyo Liboi, lakini kufika Wardeglo Dam wakatekwa nyara na inashukiwa walipelekwa Somalia.
Wazee kutoka eneo la Liboi walisema magari mawili ya wafanyibiashara hao yalionekana yakielekezwa kwenye mpaka wa Somali.
Magari hayo yalionekana mara ya mwisho eneo la Osman Baret kwenye mpaka wa Abdisugow na Gubahadhe mpakani Somalia 8.30am, polisi walisema.
Polisi walisema magari mawili yaliyokuwa na miraa yalielekezwa Somalia, wiki mbili tu baada ya al-shabaab kuteka nyara basi moja kutoka Garissa na kuwaua watu kumi wakiwemo maafisa wa polisi sita.
Al-shabaab limekuwa likidai kima cha shilingi milioni 150 baada ya madaktari wa Cuba waliokuwa wametumwa Mandera kutekwa nyara.