This archive report was first published on 11 November 2019.
Mbunge wa Laikipia Cate Waruguru amemkashifu Gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru kwa kushindwa kubeba mimba baada ya kufunga pingu za maisha.
Waruguru alisema hili wakati wa kampeni ya Inua mama katika Kaunti ya Uasin Gishu mnamo Jumapili, Novemba 10.
Alisema bado gavana huyo hajakomaa kisiasa kwani wadhifa huo ni wa kwanza.
"Wacha nimkumbushe Waiguru kuwa kwa sababu alipigiwa upato na Chama cha Jubilee, haimaanishi kuwa yeye ni Wangu Makeri wa eneo la Mlima Kenya," alisema Waruguru.
Waruguru alisema kuwa ushindi wa hivi majuzi wa Chama cha Orange Democratic (ODM), katika uchaguzi mdogo wa Kibra, haina maana kuwa BBI itafaulu.
Alimtaka gavana huyo kujiuzulu kutoka kwa wadhifa wake na kumchagua mgombeaji wa ODM kuwania kiti hicho na kubaini endapo chama hicho kitashinda.
Matamshi ya Waruguru yanakujia yapata siku tatu baada ya ODM kutwaa ushindi katika kiti cha ubunge cha Kibra baada ya Imran Okoth kuibuka mshindi.
Waiguru, mnamo Jumapili, Novemba 3, aliandama na Raila katika kampeni ya kumpigia debe Okoth eneo la Kibra.