Skip to main content

Mbinu Mpya ya Kuhifadhi Lishe inayodumu kwa Muda Mrefu

N

Nyakundi Report

Newsroom 2 min read

This archive report was first published on 2 November 2019.

Mbinu Mpya ya Kuhifadhi Lishe inayodumu kwa Muda Mrefu

Wakulima wengi wana changamoto ya kuhifadhi lishe za mifugo kwa muda mrefu, hasa wale wanaofuga ng'ombe wa maziwa. Ili kushughulikia changamoto hii, kampuni ya Packaging Industries Limited imeanzisha mbinu mpya ya kuhifadhi lishe za mifugo kwa muda mrefu.

Mbinu hii inajulikana kama 'Mama Silage Bags' na inatumiwa kuzihifadhi lishe za mifugo kwa muda mrefu, kupunguza gharama ya uzalishaji na kuboresha afya ya mifugo.

Bi Vaishali Malde, meneja wa mauzo katika kampuni hiyo, anasema kuwa mbinu hii ni bora kwa sababu haifanyi oksijeni kuwa na unyevu, na hivyo basi, lishe haziharibiki.

“Huku puya (molasses) zikitakikana kutumika kama kichocheo cha kuharakisha mchakato wa uchachukaji (fermentation) kwa mifuko mingine ya plastiki, mifuko ya ‘Mama Silage Bags’ huhakikisha kwamba sukari iliyoko kwa foda inatumika kuwa kichocheo, na hivyo kupunguza gharama ya kununua puya,” anaeleza Vaishali.

Bi Vaishali anadokeza kuwa mifuko hiyo, huzihifadhi lishe kwa muda mrefu, pasi na kupoteza virutubisho. Aidha, anasema kuwa wakulima waitumiayo mifuko hiyo huimarisha uzalishaji na kuboresha afya ya mifugo.

“Mifuko hii hudumu kwa muda mrefu, hutumika mara kwa mara, na huhifadhi kilo 600 za lishe na huuzwa kwa Sh2,000, ikilinganishwa na mifuko mieusi, ambayo huuzwa Sh800, na huhifadhi kilo 200 hadi 300 tu za lishe,” anaongeza Bi Vaishali.

Wakulima wengi wameanza kutumia mbinu hii, na wameona manufaa mengi. Geoffrey Imathew, mwenyekiti wa Naari Dairy, anasema kuwa tangu aitumie mifuko ya 'Mama Silage Bags', amepata manufaa mengi, miongoni mwayo yakiwa ni kupungua kwa gharama ya uzalishaji na muda wa kuzitengeneza lishe.

“Sinunui puya (molasses) tena, ambazo ni ghali, ambazo zingetumika kuhifadhi lishe. Pia, siwahitaji watu wengi wa kunisaidia kwa mchakato huo, kwa sababu watu wawili au watatu huhitajika tu,’’ adokeza mkulima huyo.

Jeremy Murithi, mfugaji wa ng'ombe wa maziwa katika Kaunti ya Meru, anasema kuwa ameyaona manufaa ya kuitumia mifuko ya 'Mama Silage Bags' ambapo anafichua kuwa hakuna lishe zinazoharibika maadamu mifugo hula zote, au endapo kuna uharibifu, ni kiduchu tu, ikilinganishwa na mbinu ya zamani ya kuzihifadhi lishe.

Bi Vaishali anadokeza kuwa mifuko hiyo ina rangi mbili; rangi nyeupe nje, na nyeusi ndani, na mikoba yenyewe hupanuka inapowekwa lishe, na hivyo kuzihifadhi lishe nyingi mno.

Be the first to react

Support

Support this reporting

M-Pesa support recorded against this story.

Send support →

Stay close

Get the briefing

Major updates by email. No spam.

Get email brief →

Share

Save share card

Download a clean portrait card for sharing.

Save image →