This archive report was first published on 26 October 2019.
Raila: Mswada wa BBI utapelekwa kaunti, kisha seneti na bunge ¶
Raila Odinga amesema mswada wa BBI utapelekwa kwenye mabunge ya kaunti, na kisha yale ya kitaifa. Hii inamaanisha ukikosa uungwaji mkono na kaunti angalau 24 utakuwa umekufa kama ule wa Punguza Mzigo.
Kiongozi wa ODM alisema hii Jumamosi, Oktoba 26, wakati alihudhuria mazishi ya Gumbao Jola, ambaye ni babake mdogo MCA wa wadi ya Ganda Reuben Katana.
Raila alisema wakipokea ripoti ya BBI wataunda kamati ambayo itatengeneza mswada, na kisha mswada huo kupelekwa kwenye mabunge ya kaunti na kisha baadaye upelekwe kwenye seneti na bunge la kitaifa.
"Sisi tunasema Kenya ni muhimu na lazima Kenya isonge mbele," alisema Raila.
"Mimi niliambia Uhuru sisi tuliambia watu wetu kuwa tunaenda Canaan, na hiyo safari bado iko. Lakini tumeona mto Jordan kuna mamba na ndio tunataka kuunda daraja ya kuvuka mto Jordan na ndio tuliunda BBI," aliongeza.
Raila alisema bado hawajapokezwa ripoti hiyo na kwa hivyo hakuna haja kwa baadhi ya wanasiasa kuipinga.
"Wale wengine tayari wameanza kuzunguka nchi wakisema watapinga, unapinga kitu hujui?" alisema.
"Ripoti itakuja, tutaichapisha ili wananchi wote wasome wajue iko nini pale ndani, alafu wananchi watatoa maoni yao, alafu tutaweka timu ingine ambayo itaandika ile mswada tutakayopeleka mbele ya bunge za kaunti na pia bunge," alisema.
Raila alisema pia kwamba wanasiasa wanaotaka kuipinga BBI wana kosa kwa sababu hawajui kile kinachotokea ndani ya ripoti hiyo.
"Tunataka kumaliza ugonjwa inaitwa ukabila, pili tumalize wizi ya kura...kila wakati wakenya wakienda kwa kura inaibiwa, tunataka tumalize hiyo mara hii kabisa," aliongeza.
Maelezo ya Raila ni ishara kuwa huenda mageuzi yatakayopendekezwa na timu ya BBI yakafuata mkondo uliofuatwa na Punguza Mzigo wa kupita kwa mabunge badala ya swali la kura ya maoni.