This archive report was first published on 14 October 2019.
Mauti ya Likoni feri: Familia yakana madai kuwa Mariam alisababisha ajali ¶
Familia ya Mariam Kighenda, ambaye na mtoto wake Amanda walipoteza maisha yao baada ya gari lao kuteleza kutoka kwenye feri ya MV Harambee kivukoni Likoni na kutumbukia baharini, imekana na madai kuwa mkewe alisababisha ajali hiyo.
Madai hayo yameletwa na shirika la Feri, KFS, ambalo liliweka jukumu kwa Mariam kwa kusema kwamba alirudisha gari lake nyuma bila ya kukusudia na kulisababisha kutumbukia kwenye bahari.
Hata hivyo, mumewe wa Mariam, John Wambua, amekanusha madai hayo na kusema hatahitimisha lolote hadi uchunguzi utakapokamilika.
Wambua alisema hajaelewa hadi wa sasa ni vipi gari lilirudi nyuma kwenye feri ilhali lilikuwa kwenye gia ya kuegesha.
" Gari lilikuwa limewekwa kwenye gia ya kuegesha huku breki zikiwa juu, sielewi ni vipi gari hili lilivyoteleza likiwa katika hali hiyo na kutumbukia baharini," Wambua alisema.
Tayari maafisa wa DCI wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo huku maafisa wa shirika la feri waliokuwa zamuni wakati mkasa huo ulitokea wakiwa wa kwanza kuhojiwa.
Mariam na mtoto wake mwenye umri wa miaka 4 walipoteza maisha yao baada ya gari lao kuteleza kutoka kwenye feri ya MV Harambee kivukoni Likoni na kutumbukia baharini.
Miili yao iliopolewa siku kumi na tatu baadaye na sasa inasubiri kufanyiwa upasuaji kabla kukabidhiwa kwa familia.