This archive report was first published on 4 October 2019.
Wazee wa Njuri Ncheke wameapa kuunda sheria ambayo itasawazisha mahari inayolipwa na wakazi wa Meru na Tharaka Nithi, kulingana na mkutano uliofanyika Jumatano, 2 Oktoba 2019, na Gavana wa Meru Kiraitu Murungi.
Wazee hao walikubaliana kuwa mahari imechukuliwa kama biashara na kuwaogofya vijana kufunga ndoa, na kuwa kuna mahari ghali ambayo wazazi wamekuwa wakiitisha kwa wanaume.
Wazee wa Njuri Ncheke walisema kuwa wananume wamekuwa wakikabiliwa na wakati mgumu kuwaoa wasichana kutokana na mahari ghali ambazo wazazi wamekuwa wakiitisha.
"Mume alitakiwa kumzawadi mamake binti blanketi na koti kwa baba. Siku hizi watu wanaitisha suti, viatu na bidhaa nyingine ghali mno ambazo haziambatani na desturi zetu," alisema Katibu wa Njuri Ncheke Josphat Marangiri.
Aliongeza kuwa, bidhaa hizo zenye bei ghali zinawaingiza uoga wanaume ambao wanashindwa kuoa kwa njia inayostahili.
Gavana Murungi alikubaliana na wazee hao na kuwataka kuunda sheria ambazo kila familia itastahili kufuata, akisema kuwa bei ya mahari imepanda na kuwazuia vijana kutoka Meru kuoa.