This archive report was first published on 3 October 2019.
Gavana wa Nairobi Mike Sonko ameitisha wafanyikazi wa kaunti waliofyonza hela za waathiriwa wa mkasa wa Precious Talent baada ya jamaa mmoja wa waathiriwa kusema kwamba familia zao hazijapokea hela zozote kutoka kwa kaunti.
Alisema hii kwa kujieleza kwenye ujumbe wake wa Facebook, huku akifichua kuwa waziri wa masuala ya Elimu, afisa mkuu wa fedha na afisa wa kusimamia majanga na mikasa walikuwa wamempa ripoti ya kuthibitisha familia zote zilizoathirika zilipokea KSh 100,000 kusimamia mazishi.
Aliongeza kuwa licha ya ahadi hizo zote, ni mchango wa Naibu Rais William Ruto tu umepokelewa huku familia za watoto hao zikipokea KSh 100,000 kila mmoja.
Alisema kuwa serikali ilitenga fedha za kununua masanduku manane ya wanafunzi waliofariki kando na kusimamia usafirishaji wa miili hiyo.
Alisema, "Watasema hiyo pesa walipeleka wapi. Mimi sichezi na majonzi ya familia zinazoomboleza. Lazima nitimize ahadi yangu na nitafuatilia jambo hilo kesho,".
Alitishia kuchukua hatua kali dhidi ya wafanyikazi wake iwapo uchunguzi wake utabainisha madai hayo ni ya kweli.
Alisema, "Naapa kwamba iwapo matamshi ya huyu jamaa ni ya kweli na wala sio siasa za mbunge wa eneo hilo, naona wafanyikazi wa kaunti wakielekea nyumbani,".