This archive report was first published on 26 July 2019.
Habari Zilizogonga Vichwa Vya Habari Wiki Hii ¶
Naibu Rais William Ruto alizungumzia tishio la maisha yake kwa mara ya kwanza, huku wafuasi wake wakiongozwa na seneta Kipchumba Murkomen wakikosoa uamuzi wa kiongozi wa mashtaka ya umma Noordin Haji kuagiza kukamatwa kwa Waziri Henry Rotich.
Julai 21, 2019, Naibu Rais William Ruto aliongea kwenye mahojiano na runinga ya K24, akizungumzia kuhusu kuwepo kundi linalopanga njama ya kumuua. Alisema kuwa aliweza kujadili jambo hilo na Rais Uhuru Kenyatta na hatua zinazostahili kuchukuliwa.
Wafuasi wa Ruto wakiongozwa na seneta Kipchumba Murkomen, Aaron Cheruiyot na mbunge Oscar Sudi walikosoa vikali uamuzi wa kiongozi wa mashtaka ya umma Noordin Haji kuagiza kukamatwa kwa Waziri Henry Rotich. Rotich alikamatwa Jumatatu, Julai 22, baada ya kuhusishwa kwenye wizi wa mamilioni ya pesa ya miradi ya mabwawa Arror na Kimwarer.
Julai 21, 2019, binti mmoja aliiwacha mahakama ya Kilifi ikiangua kicheko baada ya kusema alilazimika kuiba nywele za shilingi 1140 kwani alikuwa na hamu ya kuonekana mrembo kama akina dada wengine. Msichana huyo wa miaka 19 alikamatwa baada ya kuiba nywele hizo kutoka duka moja la jumla.
Julai 21, 2019, Gavana wa Kisumu Prof Anyang Nyong'o alifafanua kwa kina sababu ya bintiye Lupita Nyong'o, ambaye ni mwigizaji nguli na mshindi wa Tuzo ya Oscar kuingia na kutoka kwa siri nchini. Katika mahojiano na Citizen TV, Nyong'o alifunguka na kusema jinsi mama yake alivyowalea na jinsi anavyoilea familia yake.
Julai 2019, mwanahabari wa Citizen TV Kirigo Ng'arua alionyesha hali ya kuwa mpweke na macho yake ameyatupa kwa rapa Nyashinski almaarufu Nyas. Wiki iliyopita, mwanamuziki huyo alikuwa kwenye mkutano na wanamuziki wenzake wakiwamo; Nameless, Bien Aime, Size 8, Ringtone, Otile Brown na ni kutokana na picha iliyotupwa mtandaoni ndipo Kirigo alipoirusha ndowano yake.