This archive report was first published on 19 July 2019.
Ekuru Aukot: Maisha Yangu Yamo Hatarini Baada ya Vamizi Kuivamia Afisi Yangu ¶
Ekuru Aukot, mgombea wa Urais wa chama cha Thirdway Alliance, amedai kwamba maisha yake yamo hatarini baada ya wahuni kuivamia afisi yake ya Lavington Alhamisi, 18 Julai usiku.
Aliongeza kwamba anatafuta mbinu ya kukutana na kufanya mazungumzo na Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai.
Alidai kwamba wanaume sita walioficha nyuso zao walivamia afisi yake mida ya saa mbili usiku, na walitoweka na kipakatalishi na simu ya rununu ya Katibu Mkuu wa chama hicho Fredrick Okango.
Aliongeza kwamba uchunguzi uliofanywa kwa sasa umeonyesha kwamba shambulizi hilo lilikuwa la uhalifu wa kawaida, na wala majambazi hao hawakuwa na nia ya kumdhuru Aukot wala wandani wake.
Aliongeza kwamba majangili hao walitumia mwanya nyuma ya afisi hiyo na kupenyeza hadi afisini humo kwa kuwa ujenzi bado unaendelea katika jengo hilo.
Maoni ya Aukot yalijiri siku moja tu baada ya Tume ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC) kuiidhinisha kampeni yake kushinikiza kura ya maoni ya kurekebisha katiba.
IEBC ilitangaza kuwa kampeni hiyo ya Punguza Mzigo ilipata saini zaidi ya milioni moja kama inavyohitajika kisheria kuafiki lengo hilo.