Madai ya Naibu Rais William Ruto kuhusu kuwepo kwa njama ya wizi wa kura za urais kunaonekana kuhatarisha matokeo ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanaonya kuwa, madai hayo yatasababisha wapigakura katika ngome za Naibu wa Rais kukata tamaa na kukataa kujitokeza kupiga kura Agosti 9.
Alhamisi, Dkt Ruto alidai kuwa IEBC imeyaondoa majina 800,000 ya wafuasi wake kutoka kwenye orodha ya wapiga kura, na kuwaweka kwenye ngome.
Alisema wataandikia IEBC waraka kuhusu suala hilo, akisema, tume hiyo lazima ihakikishe kuwa uchaguzi unaendeshwa kwa haki na njia huru.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alikashifu matamshi ya Dkt Ruto, akisema kuwa sajili ya IEBC haijavurugwa wala hakuna jina la mpiga kura ambalo limeondolewa.
Alipewa fursa ya kujibu, Bw Chebukati alikiri kuwa baadhi ya maafisa wa tume hiyo walihamisha majina ya wapigakura kutoka kituo kimoja hadi kingine bila idhini yao, na akaahidi watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Wadadisi wanasema kauli ya Dkt Ruto huenda ikamponza na inaonyesha kuwa amekosa imani katika utendakazi wa IEBC, tume ambayo alisifu 2017 akisema iliandaa uchaguzi huru waliposhinda hatamu yao ya pili pamoja na Rais Uhuru Kenyatta.
“IEBC ina makamishina ambao hawatoki kabila moja na ni vigumu sana waafikiane kuwa majina ya watu wa kabila fulani, yaondolewe katika sajili ya wapigakura. Naibu Rais anawatayarisha wafuasi wake kisaikolojia wakatae matokeo ya uchaguzi,” alisema Martin Andati, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.
“Kauli hiyo inaweza kumponza hasa eneo la Kati ambako amekuwa na uungwaji mkono tangu 2017. Wakazi huenda wakaamua kutoshiriki uchaguzi wakisema ushaamuliwa na kura zao hazitakuwa na umuhimu wowote ikizingatiwa mara hii pia hawana mwaniaji maarufu ambaye anaweza kutwaa urais kutoka eneo hilo,” akaongeza.
“Yamkini Naibu wa Rais Ruto anafahamu kuwa madai ya wizi wa kura yanakatisha tamaa wafuasi wake. Hiyo ndiyo maana analalamika na kisha kukimbia katika mikutano ya kampeni kuwahakikishia kuwa kura zake haziwezi kuibwa,” anasema Javas Bigambo, mdadisi wa masuala ya siasa.