This archive report was first published on 6 January 2022.
Hasara Tele Wanabiashara Wakitorokea Eneo Salama ¶
Ukosefu wa usalama eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa unatia hasara kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara katika kaunti zinazokumbwa na hali hiyo.
Wafanyabiashara kadhaa katika kaunti za Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet na Baringo wamefunga biashara zao na kutoroka eneo hilo kufuatia mashambulizi mapya ambayo yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 10 katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.
Shule zilizo karibu na kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet pia zimeathiriwa na mashambulizi ya kulipiza kisasi, na baadhi ya familia zimehamia maeneo salama.
“Shule nyingi huenda zikose kufunguliwa kutokana na hali ya usalama. Tunataka usalama kuimarishwa katika taasisi za masomo,” alisema mbunge wa Sigor Peter Lochakapong.
Maafisa wa utawala na usalama katika eneo hilo wanakiri kwamba wahalifu wanaotekeleza mashambulizi hayo bado hawajakamatwa, ishara ya uwezekano wanapanga mashambulizi zaidi.