This archive report was first published on 6 January 2022.
Waziri wa Elimu katika Kaunti ya Nyeri, Sabina Aroni, amesema kwamba serikali haitawashurutisha walimu wakuu wa shule kuhusu utaratibu watakaotumia wanapoitisha karo kutoka kwa wazazi.
Badala yake, usimamizi wa shule utahitajika kujadiliana na wazazi binafsi kuhusu mbinu wanazopanga kutumia kulipa masalio ya karo bila kutatiza uendeshaji wa huduma muhimu shuleni.
Alisema kuwa licha ya tangazo la hivi majuzi lililotolewa na Waziri wa Elimu, Profesa George Magoha, akishauri shule kutowafukuza wanafunzi kwa kukosa karo, mpangilio kama huo unaweza tu kufuatwa baada ya majadiliano ya kina baina ya wahusika.
“Shule zinahitaji pesa ili kuendelea na ikiwa wazazi hawatalipa tutaendeshaje shule zetu?” aliuuliza afisa huyo.
Alisema kuwa pesa bado ni kiungo cha kimsingi katika uendeshaji wa shughuli za taasisi za elimu.
“Ikiwa maji na umeme utakatwa, chakula kikose kulipiwa, hilo ni tatizo kuu na huo ni wajibu wa wazazi na walimu wakuu. Hatuingilii kamwe mpangilio huo na hivyo basi acha kuwe na maafikiano kuhusu ni vipi watashughulikia hayo,” alisisitiza.
Waziri Aroni alisema hii mwezi Januari 6, 2022, katika taarifa yake ya kwanza kuhusu suala hilo.