This archive report was first published on 1 January 2022.
Bei ya unga wa mahindi inaendelea kuwa na hofu ya kuongezeka baada ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) kuongeza bei ya kununua mahindi kutoka Sh2,700 hadi Sh3,000 kwa gunia moja la kilo 90.
Hiyo ina maana kwamba kampuni za kusaga unga wa mahindi zitalazimika kununua mahindi kwa bei ya juu, hali itakayochangia kuongezeka kwa bei ya unga kwa zaidi ya bei ya sasa ya Sh120 kwa pakiti ya kilo mbili madukani.
Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya, anaweza kuwakinga Wakenya kutokana na ongezeko la bei ya unga kwa kuingilia kati na kuhakikisha kuwa kampuni za kusaga unga zinauziwa mahindi kwa bei nafuu.
Wakati wa kuwasilisha taarifa kwa Bunge la Taifa mnamo 2018, mtangulizi wake, Mwangi Kiunjuri, aliamuru NCPB ipewe ruzuku ya Sh6 bilioni kutoka kwa Hazina ya Kitaifa kuiwezesha kupunguza bei ya mahindi kwa kampuni za kusaga unga.
Hatua hiyo ilichangia kushuka kwa bei ya unga kutoka Sh150 hadi Sh75 kwa pakiti ya kilo mbili.