This archive report was first published on 1 November 2021.
Na Leah Makena, Keroka, Kisii
Mama wa hapa alishangaza wengi alipokataa kupeana zawadi kwa maharusi na kurejea nyumbani kwa kukosa chakula sherehe ya harusi.
Alipokuwa jirani ya binti aliyekuwa na harusi, mama alikuwa akihudhuria mikutano ya harambee na kuchangia pakubwa kufanikisha harusi hiyo kando na kununua zawadi ya sufuria mbili alizobeba ili kukabidhi wanandoa.
Sherehe iliendelea ilivyotarajiwa hadi jioni, wakati waliohudhuria walipoagizwa kujipanga ili wapate chakula.
Alipokataa kufuata utaratibu na kujiunga na upande wa wazazi, mama alisema kwamba alikuwa mtu wa maana kwa kidosho.
“Tulikuwa tumeonyeshwa wazazi wa pande zote mbili na hao pekee ndio wanatumia meza spesheli. Hao wengine wanapewa chakula kutoka upande wa pili. Hatutaki msongamano upande huu kwa sababu ni muhimu kuheshimu wazazi wa maharusi,” mmoja wa wapishi alieleza.
Alipoulizwa kuhusu hali hiyo, mama alisema, “Kwa nini nitoe zawadi na nimebaki nikiwa njaa pekee yangu? Sasa nimepata matokeo ya kujishughulisha kwa muda mrefu kwani hata niliowashughulikia leo hawanitambui. Nitatumia sufuria kupikia kwangu, hata sikuwa na za kutosha jikoni.”