This archive report was first published on 28 October 2021.
Kilimo Kwa Ajira: Mwanafunzi Akiwa Chuo Kikuu Anajitosa Katika Ukulima ¶
Na WINNIE ONYANDO
Uyawi, Kaunti ya Siaya, 28 Oktoba 2021 - Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Jaramogi Oginga Odinga, Rueben Onyang'o, anakusanyika mapato kutokana na ukulima na kuendelea na masomo yake.
Onyang'o, 22, ana shamba la robo ekari ambalo lina sukuma wiki, nyanya, na matikitimaji. Anasema kuwa alipenda ukulima tangu akiwa mdogo na alianza baada ya kumaliza Kidato cha Nne.
Alipokosa msaada wa karo ya kujiunga na Chuo Kikuu, Onyang'o aliamua kujitosa kabisa katika ukulima. Maarifa katika ukulima aliyopata kutoka kwa hayati baba yake miaka mingi iliyopita yalimpa ujasiri wa kuanza ukulima katika shamba lao lililo kwenye ufuko wa Ziwa Victoria.
"Nilitafuta njia ya kupata aghalau karo ya kujiunga na Chuo Kikuu. Baada ya kukosa msaada kutoka kwa marafiki, niliamua kujitosa kabisa katika ukulima. Tayari nilikuwa na ujuzi katika sekta hiyo na hivyo nikaanza kazi mara moja," asimulia Onyang'o.
Onyang'o anatumia takriban Sh50,000 katika maandalizi ya shamba kabla ya kuanza kupanda. Kila mwaka, anavuna mara tatu kutoka shambani mwake. Sukumawiki humpa Sh10,000 kwa wiki, nyanya humpa faida ya Sh100,000 huku tikiti maji kumpa Sh40,000 katika kila kipindi cha mavuno.
Shamba lake linapatikana katika ufuko wa Ziwa Victoria hivyo basi wanyama kama vile viboko hulivamia shamba lake na kula mimea yake. Onyang'o anaeleza kuwa anahusisha mapato duni na ukosefu wa maarifa na kutotumia dawa za kisasa kama vile mbolea aina ya Haifa MPK, Calcium Amonium Nitrate (CAN) na dawa ya kuboresha ukuaji kama vile Vegimax, matumizi ya Topaz na Co-power.