This archive report was first published on 26 July 2021.
Wanawake wa Balagha Wanaeleza Mahangaiko Yao ya Kupata Matibabu ¶
Wanawake kutoka kijiji cha Balagha, Kaunti ya Kilifi, wanaeleza kwa uchungu kuwa hawana kituo cha afya kilichoko karibu na wao, na hulazimika kwenda kwa mwendo mrefu kutafuta huduma za kimatibabu.
Wanawake hao wanaendelea kudondoa mboga za mchunga huku wakipiga gumzo, na gumzo lao lilihusu sana mashaka wanayopitia katika harakati za kutafuta matibabu katika eneo hilo.
Bi Kajeni Menza, mmoja wa wanawake hao, alisema kuwa shida yao ni kuwa hatuna hospitali, na tunateseka sana tukiwa wagonjwa na mara nyingi inakuwa shida kwetu kusafiri zaidi ya kilomita 15 kutafuta matibabu.
Bi Menza alisema kuwa kutoka kijiji cha Balagha hadi katika zahanati ya Matolani kunagharimu Sh500 kwa bodaboda kwa mwendo mmoja, na wanawake wajawazito wameathirika pakubwa wanapotaka kujifungua hali inayowalazimu kutegemea wakunga wa kienyeji ambao pia hawapatikani kwa urahisi hasa wakati wa usiku.
Wanawake hao hulazimika kwenda kwa mwendo mrefu kutafuta matibabu, na mara nyingi hukosa huduma za afya bora, na hata baada ya kujifungua hawapeleki watoto wao kupata chanjo.
Bi Josphine Ngala alisema kuwa hali mbovu ya barabara iliyojaa mabonde na miteremko imekuwa tatizo kubwa kwa wakazi hao, na wanawake wengi huwa katika hatari ya kupoteza maisha wanapoenda hospitalini.
Bi Ngala alisema kuwa mambo huendelea kuwa magumu kwa wanawake ambao hupata matatizo na kuwalazimu kwenda kujifungua katika hospitali ya Malindi, hasa kutokana na shida ya usafiri.