This archive report was first published on 12 July 2021.
Uchumi wa kilimo ni muhimu sana nchini Kenya, na kuna changamoto nyingi zinazokabili wakulima wengi. Hata hivyo, kampuni moja jijini Nairobi, NatureLock, imezindua kiwanda cha kuongeza thamani ya mazao mabichi ya kilimo, hasa ya hadhi ya chini na yanayokataliwa sokoni.
Bi Tei Mukunya, Afisa Mkuu Mtendaji wa NatureLock, anasema kwamba kampuni yao inalenga kuokoa mazao ya shambani yanayopotea baada ya mavuno. "Tunaleta pamoja mazao ambayo yangeoza, kwa kuyafunga yadumu muda mrefu. Tunayaongeza thamani kwa kutumia malighafihai," anasema.
Bi Tei anasema kwamba wamekumbatia mifumo ya Kisayansi kuyakausha. "Shabaha yetu ni kuokoa mazao yanayokataliwa shambani ilhali ni bora. Kwa mfano, karoti zilizovunjika, vitunguu vinavyoonekana kutokuwa na umbo la kuvutia (maumbile), nyanya, viazi, kati ya mazao mengineyo, ambayo hayapati soko la haraka," anafafanua.
Ulimwenguni, thuluthi moja ya chakula hupotea, watu wengi wakiendelea kusalia njaa. Kulingana na Bw Marteen Brouwer, Balozi wa Uholanzi nchini Kenya, haja ipo sekta ya kilimo na biashara kuwa na miakati bora, ili kudhibiti vyakula kuharibika. "Serikali inahitaji kuweka mipango na mikakati maalum," Balozi huyo akahimiza, akiahidi kwamba serikali ya Uholanzi itashirikiana na NatureLock.
Bi Tei Mukunya anasema kwamba kiwanda hicho kiligharimu zaidi ya Sh40 milioni, na kina wafanyakazi 28. "Tunapanga kuwa na viwanda vitano kufikia mwaka ujao. Vile vile, tunalenga programu za kulisha shule," afisa huyo akasema.
Alisema kufikia sasa wana vituo sita vya kukusanya mazao.