This archive report was first published on 19 July 2020.
Wasanii Wahamasisha Wakenya Wajikinge Dhidi ya Janga la Corona ¶
Waimbaji wengi wa Kenya wamejitolea kuimba nyimbo za kuwasihi wananchi wajikinge na janga la corona. Nyimbo hizi zina lengo la kuwahamasisha wananchi wajichunge na yasiyotakikana kuyafanya wakati huu.
Msanii wa Injili, Doris Owino, amesema kuwa yuko karibu kuimba wimbo unaohusiana na maradhi hayo ya corona lakini anasubiri kuukamilisha ili aupe jina litakalolingana na wakati huo atakapokuwa anauzindua.
"Kwetu sisi waimbaji tuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha tuanajitosa kuimba nyimbo za kuwasihi Wakenya wajilinde na janga hili ambalo ni la kitaifa. Tunaimba kuwahamasisha wananchi wajichunge na kujiepusha yasiyotakikana kuyafanya wakati huu," amesema Doris.
Msanii mwingine, Dianah Dinah, amesema wana wajibu mkubwa kuimba nyimbo za mada za ugonjwa wa Covid-19 kwa njia zote kuanzia kwa athari zake pamoja na kujikinga kuepuka maambukizi hasa kwa kuwa bado unazidi kusambaa hapa nchini.
"Tunawajibika kutuma jumbe kwa Wakenya wajihadhari na wafuate yale yanayohitajika kuzingatiwa wakati huu ugonjwa huu unazidi kutambaa na kuathiri familia kadhaa," amesema Dinah.
Msanii mwingine, Brother Nassir, amesema kuwa amefikisha ujumbe muhimu kwa wale wanaopenda muziki na amefurahi kwa kuwa ujumbe wake umeanza kuenezwa kwenye magari ya matatu, tuktuk na majumbani.
"Tuko katika hatari ya janga la corona hivyo nimeona nina wajibu mkubwa wa kutuma ujumbe ambao nina hakika umewafikia wengi na utazidi kuwafikia wengine ili uweze kukabilika ipasavyo na utoweke na maisha yarudi kama yalivyokuwa hapo awali," amesema Nassir.
Waimbaji wengine wanaojitayarisha kuimba nyimbo zinazohusiana na corona ni pamoja na wale wa maeneo ya Kaunti za Kilifi, Taita Taveta na Kwale.