This archive report was first published on 15 July 2020.
Julai 14, 2020, jamaa mwenye umri wa makamo kutoka Kakamega alipatikana ameaga duni katika gari la kibinafsi katika soko la Amalemba, Kakamega.
Walioshuhudia kisa hicho walisema kwamba walimpata jamaa akiwa angali hai ijapokuwa alikuwa akipumua kwa umbali walipolifungua gari hilo.
Walishindwa kumsaidia kwa kuwa hakuwa na maski na walihofia huenda alikuwa akiugua COVID-19, kama ilivyoripotiwa na K24 Digital.
'Polisi walipofika eneo alilokuwa baada ya dakika 30 walimkuta tayari amekata roho,' mkazi mwingine alisema.
Alionekana akielekea upande wa Vihiga kutoka Kakamega na alipofika katika soko hilo aliliegesha gari hilo majira ya saa kumi unusu jioni na wala hakusonga tena.
Mwili wa marehemu ulipelekwa katika makafani ya hospitali ya rufaa ya Kakamega huku uchunguzi wa kilichomuua ukianzishwa.
Alitambulika kama mfanyikazi katika afisi ya maonesho ya kilimo ambaye alikuwa akisimamia kuandaa hafla za kila mwaka kaunti ya Kakamega.