This archive report was first published on 5 August 2019.
Ken Okoth: Mama yake marehemu hakutaka mwili wa mwanawe kuteketezwa ▷ Kenya News ¶
Angeline Ajwang', mama ya Mbunge wa Kibra, Ken Okoth, alijaribu kuzuia mwili wa mwanawe kuteketezwa baada ya kifo chake kwa saratani. Hata hivyo, mke wa Okoth, Monica, alisisitiza kuwa mwili wa marehemu uliteketezwa kwa sababu ilikuwa ni mapenzi yake iwe hivyo.
Okoth alikuwa Mbunge wa Kibra na alifariki Alhamisi, Julai 25, baada ya kuugua saratani. Mwili wake uliteketezwa asubuhi ya Jumamosi, Agosti 3, Keriokor, jijini Nairobi, bila ya mama yake mzazi kushuhudia.
Angeline Ajwang' alijaribu kuzuia shughuli hiyo bila ya mafanikio. Aliwapigia viongozi kutoka jamii ya Waluo lakini hamna aliyemsaidia kuzuia kuteketezwa kwa mwili wa mwanawe.
Baraza la Wazee wa jamii ya Waluo pia ilisikitishwa mno na hatua ya kuuteketeza mwili wa Ken. Walitaka uzikwe kawaida ya mila na desturi za jamii hiyo.
Wazee hao walisema Monica ni lazima kujitokeza wakati wa tambiko, shughuli itakayofanyika Kabondo, Homa Bay. Sehemu ya tambiko hizo ni urithi wa Monica kwa kuzingatia mila za jamii ya Waluo.
Angeline Ajwang' na baadhi ya watu wengine wa familia hawakuhudhuria hafla ya kuuteketeza mwili inayodaiwa kufanyika 3am, Jumamosi, Agosti 3, Keriokor jijini Nairobi.
Elvis Oluoch, mpwa wake Okoth, alisema mama ya marehemu hakufahamu lolote kuhusu kuteketezwa kwa Okoth hadi baada ya shughuli hiyo kukamilika.
Ingawa mjane wa marehemu alishikilia ni kwa ajili ya kutimiza mapenzi ya mume wake, familia ilikataa na kusema mwili ulifaa kupelekwa nyumbani kwao Kaunti ya Homa Bay uzikwe.