This archive report was first published on 29 June 2019.
Mnamo Juni 29, 2019, wakaazi wa Kaunti ya Taita Taveta walieleza wasiwasi wao kuhusu kuongezeka kwa idadi ya wanyama pori wanaovamia maboma yao. Miezi miwili iliyopita, msichana wa miaka 11 aliuawa na jamaa zake kupata majeraha makubwa baada ya kuvamiwa na simba nyumbani kwao.
Wakaazi wanasema kwamba hakuna usaidizi wowote wamepokea hadi sasa, na kwamba wanyama pori wamekuwa kero katika eneo hilo. Ndovu wameripotiwa kuvamia mashamba ya wakaazi na kuharibu mimea shambani, na wakati mwingine kuwavamia watu na kuwakanyaga kanyaga hadi kufa.
Lakini zaidi ya hayo, ajuza mmoja aliyezungumza na TUKO.co.ke alisema kwamba zamani palikuwapo na tambiko zilizofanywa na wazee wa vijiji ili kuzuia wanyama pori kuingia na kuvamia shamba au mifugo. Angelina Wakesho alisema, “Wahenga walinena mwacha mila ni mtumwa, na kwa jamii yetu hii tumepoteza wapendwa wetu, vyakula mashambani, na mifugo kwa kuwacha mila.”
Wakesho aliendelea kusimulia jinsi tambiko hizo zilikuwa zilikifanywa, “Nyayo za wanyama pori hao zingechukuliwa na mwanamke au mwanamume aliyefunga kuzaa, kwa kutumia panga isiyokuwa na mpini. Hatimaye, nyayo hizo hungewekwa kwenye nyumba ya konokono, na dawa za kienyeji.”
Kwa upande wake, Maureen Chari ambaye ni mkazi wa Mwatate alisema kwamba ingawa yeye ni mwokovu, anaaminia kwamba kuna wakati hasidi anaweza kukuendea kinyume na kukutumia wanyama pori nyumbani kwako ili wakudhuru, “Kuna kipindi nilikosa kutoka nje kwa wiki moja baada ya ndovu kukita kambi nje ya nyumba yangu. Ilibidi washirika wa kanisa wafunge na kuomba kwa ajili ya tukio hilo ndipi wakaondoka. Roho ea Mungu alimnenea mchungaji wetu na kuonekana sio jambo la kawaida, ndovu hao walikuwa wametumwa kwangu.”