Mapema mwezi Mei, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani walizungumza na Rais Vladimir Putin wa Urusi kwa zaidi ya dakika 80 kwa njia ya simu, wakiomba kufanya mazungumzo ya kina na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine kama njia moja ya kumaliza mzozo kati ya nchi hizo mbili.
Waliomba hivyo kwa sababu ndiyo njia pekee ambapo mzozo huo utapata suluhisho la kudumu, kwa kusema kwamba Putin lazima asititie mashambulio yake dhidi ya Ukraine na kuondoa majeshi yake nchini humo mara moja.
Putin alisema kuwa Urusi iko tayari kurejelea mazungumzo kati yake na Ukraine kama ilivyokuwa hapo awali, lakini haikueleza uwezekano wa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Zelensky.
Awali, Zelensky alisema hakuwa tayari kufanya mazungumzo na Putin, lakini akaeleza kuhusu haja ya kumaliza mapigano hayo.
Wajumbe tofauti kutoka nchi hizo mbili wamekuwa wakifanya mazungumzo kumaliza mzozo huo bila mafanikio tangu Februari vita kati ya nchi hizo vilipoanza.
Urusi ilifanya msururu wa mashambulio makali katika kiwanda cha kutengeneza vyuma cha Azovstal, jijini Mauripol, na kwa hivyo mataifa hayo mawili yalimrai Putin kuwaachilia wapiganaji 2,500 wa Ukraine iliowakamata katika kituo hicho.