Kigoda cha Pwani: Raila na Ruto kutumia ardhi kama chambo cha kampeni ¶
Na Philip Muyanga
Chini ya siku sabini kabla ya uchaguzi wa Agosti 9, kampeni za kisiasa katika ukanda wa Pwani zinatarajiwa kuonekana kwa kasi baada ya wagombea wakuu wawili wa urais Dkt William Ruto na Bw Raila Odinga kutaja vikosi vitakavyoendeleza kampeni zao ukanda huo.
Ukanda wa Pwani ni mojawapo ya maeneo yanayoshuhudia kampeni zilizoko na joto jingi la kisiasa, na wawaniaji wengi hususan wale wa urais hutumia swala la ardhi, ambalo huzua hisia kali miongoni mwa wananchi.
Wachanganuzi wa kisiasa wanaotajwa katika vikosi vya kampeni za viongozi hao wa muungano wa Kenya Kwanza na ule wa Azimio wanaonyesha kuwa kwa sasa ndio mkoko umealika maua.
Magavana Salim Mvurya na Amason Kingi wanaongoza kikosi cha Bw Ruto, pamoja na aliyekuwa gavana wa Lamu Issa Timamy na mwakilishi wa wanawake katika bunge kutoka kaunti ya Taita Taveta Bi Lydia Haika.
Watapambana na kikosi cha muungano wa Azimio la Umoja, ambacho kinaongozwa na Gavana Hassan Ali Joho pamoja na mwenzake wa Taita Taveta Granton Samboja, mbuge wa Mvita Abdulswamd Shariff Nassir na mwenzake wa Taveta Bi Naomi Shabaan na mfanyibiashara Suleiman Shahbal.
Maana yake, vikosi hivyo vya kampeni vinatarajiwa kupatia viongozi wao takriban kura 1.9 milioni kutoka kaunti zote sita za Pwani.
Swala la ardhi ni mojawapo ya maswala yanayotarajiwa kuangaziwa na viongozi hao, pamoja na swala la uchumi wa bahari na ugavi wa mamlaka ya kisiasa.
Naibu rais William Ruto alisema kuwa iwapo atachukua hatamu za uongozi wa nchi, atakuwa na mfuko wa hazina maalum ya kutafuta pesa za kununua shamba ili kutoa kwa maskwota.
“Ni nini yeye (Bw Odinga) amefanya kutatua shida hiyo? Ilikuwa wakati wake kama waziri mkuu ndiposa swala la unyakuzi wa ardhi lilikuwa kubwa,” alidai Dkt Ruto.
Aliongeza kusema kuwa Bw Odinga hakuangazia swala la ardhi alipokuwa mamlakani.