This archive report was first published on 1 July 2019.
Umaarufu wa chama cha upinzani cha ODM umefifia, kwa mujibu wa kura ya maoni ya Infotrak. Kura hiyo ilionyesha kwamba asilimia 21 pekee ya wakenya kinaunga mkono chama hicho.
Ukiondoa wafuasi wa chama hicho, asilimia 31 ya wakenya walisema ODM kilisahau kazi yake ya kuipiga msasa serikali na badala yake kikaanza kushiriki urafiki wa karibu na chama kinachoongoza.
Angela Ambitho wa Infotrak alisema, "Wakenya wanahisi mwangalizi wa serikali yuko usingizini na kusahau kazi yake. Hiyo imeonekana kwa ODM kuungwa mkono na asilimia 21 pekee."
Umaarufu wa chama cha ODM umefifia tangu Raila Odinga afanye makubaliano na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi 9, 2018. Chama hicho kilipunguza makali yake katika kuipiga msasa serikali.
Wanachama wa ODM wamebakia bubu au mashabiki wakupigia debe misimamo ya serikali ya Jubilee. Hii ni tofauti na hapo awali ambapo wanachama wake walikosoa vikali serikali pamoja na miradi yake.
Umaarufu wa chama cha Jubilee kilichoko serikalini unazidi kutamba huku asilimia 40 ya wakenya wakisema kiko ngangari.